BILA kujali umri wako, unahitaji kufanya mazoezi kwa ukawaida ili uwe na afya nzuri. Watu wengi leo hawafanyi mazoezi ya kutosha. Kwa nini ni muhimu kufanya mazoezi? Kwa sababu kufanya mazoezi kunaweza kukusaidia:
Kulala vizuri.
Kuweza kutembea kwa wepesi.
Kuwa na mifupa na misuli yenye nguvu.
Kudumisha au kuwa na uzito wa mwili unaofaa kiafya.
Kupunguza hatari ya kuwa na ugonjwa wa kushuka moyo.
Kupunguza hatari ya kufa mapema.
Ikiwa haufanyi mazoezi, huenda ukapatwa na:
Ugonjwa wa moyo.
Ugonjwa wa kisukari aina ya 2.
Kupatwa na shinikizo la damu.
Mwili kuwa na kiwango cha juu cha kolesteroli.
Kupatwa na kiharusi.
Kwa kuwa mazoezi yanayofaa yanategemea umri na afya ya mtu, ni vizuri kuwasiliana na daktari wako kabla ya kuanza kufanya mazoezi yoyote mapya. Kulingana na mapendekezo mbalimbali, watoto na vijana wanapaswa kutumia angalau dakika 60 kila siku kufanya mazoezi rahisi na magumu. Watu wazima wanapaswa kutumia dakika 150 za mazoezi rahisi au dakika 75 za mazoezi magumu kila juma.
Fanya mazoezi utakayofurahia. Unaweza kucheza mpira wa kikapu, tenisi, mpira wa miguu, kutembea haraka, kuendesha baiskeli, kulima bustani, kukata kuni, kuogelea, kupiga kasia mtumbwi, kukimbia polepole, au mazoezi yoyote ya viungo. Utajuaje kwamba mazoezi ni rahisi au ni magumu? Kwa ujumla mazoezi rahisi hukufanya utoe jasho, lakini magumu ni yale ambayo unapoyafanya inakuwa vigumu kwako kuzungumza.
No comments:
Post a Comment