Koo la chakula ni kiungo kama bomba kinachounganisha mdomo na tumbo la chakula. Kinafanya kazi ya kupitisha chakula kutoka mdomoni kwenda tumboni. Koo la chakula linaukubwa wa sentimeta 25 kwa mtu mzima. Katika kiungo hiki uvimbe wa saratani unaweza kukua mahali popote. Na uvimbe huu unapokua unaweza kuathiri misuli ya ndani na misuli ya koo lenyewe.
Kweli kuhusu saratani ya koo la chakula
Inashika nafasi ya 9 katika orodha ya aina ya saratani inayowapata watu duniani. Huku nchi zinazoendea zikiongoza.
Wagonjwa wengi hawana dalili yoyote, lakini baadaye huonesha dalili baada ya saratani imeshaenea katika maeneo mengi ya mwili.
Uwezekano wa kupona baada ya kugundulika katika hatua hii ni 10% tu. Yaani mtu 1 kati ya watu 10 ndio wanaweza kupona.
Mara nyingi saratani ikikaa kwa muda bila kugundulika huenea kwenye ini, mapafu na maeneo yanayozunguka mapafu, mifupa, na tezi ya adrenali.
Aina za saratani ya koo la chakula
Adenocarcinoma
Hii huathiri tezi zinazozalisha uteute kwenye koo la chakula. Mara nyingi hutokea sehemu ya chini ya koo la chakula. Ni aina ya saratani inayowaathiri zaidi wazungu.
Squamous cell carcinoma
Aina hii huathiri chembechembe hai bapa za koo la chakula. Mara nyingi hutokea sehemu ya juu na ya kati ya koo la chakula. Ni aina ya saratani iliyoenea maeneo mengi zaidi duniani.
Sababu ya saratani ya koo la chakula
Kama ilivyo kwa saratani nyingi, chanzo chake halisi hakifahamiki. Lakini inaaminika kuwa mabadiliko ya vinasaba vya chembechembe hai za koo la chakula zinafanya chembechembe hizo kuzalishwa kwa wingi sana kuliko chembechembe za kawaida. Mabadiliko haya hupelekea chembechembe hizo kushindwa kupokea taarifa ya amri ya zenyewe kufa. Hivyo zinajazana na kusababisha uvimbe wa saratani.
Vitu vinavyoongeza uwezekano wa mtu kupata saratani ya koo la chakula
Kinachoweza kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya koo la chakula ni:
Upungufu wa matunda na mbogamboga katika mlo. Hii husababisha upungufu wa vitamin A, B6, C, riboflavin, thayamini,[1] upungufu wa madini ya zinki[2]
Pombe
Tumbaku na uvutaji
Magonjwa ya fangasi
Mazingira ya mjini (mazingira machafu)
Virusi vya HPV
Uwepo wa chembechembe hai kwenye koo la chakula zilizoanza kubadilika (barrett’s esophagus)
Kuwepo kwa tatizo la ugumu wa kumeza kutokana na misuli ya mlango wa koo la chakula kwenda tumboni hailegei vizuri (achalasia)
Tabia ya kula na kunywa vyakula na vinywaji vya moto sana[3]
Tiba ya mionzi katika kifua au sehemu ya juu ya tumbo
Kuwa na uzito mkubwa
Tatizo la kurudisha chakula kutoka tumboni kurudi kwenye koo la chakula (gastroesophageal reflux, GERD)
Watu waliokatika hatari zaidi ya kupata saratani ya koo la chakula
Wanaume wako katika hatari x3 zaidi. Uwezekano wa kupata saratani ya koo la chakula ni 75% na wanawake ni 25%.
Umri mkubwa; miaka 50+ wako katika hatari zaidi
Waamerika wenye asili ya kiafrika wako katika hatari zaidi kuliko jamii nyingine.
Dalili za saratani ya koo la chakula
Mwanzoni mwa kuibuka kwa saratani hii unaweza usisikie dalili yoyote. Lakini kadri inavyoendelea utaanza kusikia dalili zifuatazo:
Kupungua uzito
Kutematema mate mengi mara mara
Upungufu wa damu (pernicious anemia)
Maumivu ya tumbo baada ya kula
Mgonjwa anaweza kupata shida ya kuharibika sauti kwa sababu ya kurudi kwa tindikali ya tumbo kwenye koo. Matone ya tindikali ynayosababisha radha mbaya yanaweza kuunguza misuli inayotoa sauti na hivyo kuharibu sauti.
Chakula kutosagika vizuri (matatizo sugu ya kushindwa kusaga chakula vizuri)
Chembe ya moyo (maumivu ya kuungua karibu na moyo/kifuani)
Maumivu au ugumu wakati wa kumeza, mara nyingi unahisi kama kuna kitu kinakwama kwenye koo au kifuani.
Kubanwa/kukabwa mara kwa mara wakati unakula
Kutapika damu.
Chakula kurudi kwenye koo la chakula kutoka tumboni
Maumivu ya sehemu ya chini ya kifua au sehemu ya juu ya tumbo. Kama saratani imeenea maeneo mengine maumivu yanaweza kuwa maeneo ya kifua au mgongoni.
Uchovu
Kikohozi sugu
kwikwi
Vipimo vya saratani ya koo la chakula
Endoscopy; hii inahusisha kifaa chenye kamera iliyofungwa mbele ya kibomba chembamba ambacho kinaingizwa kwenye koo na kuruhusu daktari kuona ukuta wa ndani wa koo la chakula kuona kama kuna shida yoyote.
X-ray
Biopsy; ni kitendo ambacho daktari anachukua sehemu ya uvimbe kwa msaada wa endoscopy na kupeleka maabara kwa ajili ya vipimo.
CT scan, PET scan au MRI hutumika kuangalia kama saratani imeenea katika maeneo mengine ya mwili.
Lini umwone daktari?
Unapoona dalili yoyote katika zilizotajwa hapo juu inayoendelea zaidi na kukutia wasiwasi, omba kukutana na daktari akusaidie.
Madhara ya saratani ya koo la chakula
Kama saratani ya koo la chakula itaendelea zaidi, madhara haya yanaweza kutokea
Kuziba kwa koo la chakula. Saratani inaweza kufanya kuwa vigumu au kushindikana kabisa kumeza vyakula au vinywaji.
Maumivu makali
Kuvuja damu kwenye koo la chakula. Japokuwa inaweza kuanza taratibu, inaweza ikaja ghafla na ikatoka nyingi sana wakati fulani.
Matibabu
Mara ntingi tiba ya mionzi huambatana na dawa. Madhara yake ni makubwa zaidi kama njia zote mbili zikitumika kwa pamoja. Madhara yake ni pamoja na
Ngozi kuonekana kama imeungua
Maumivu au ugumu wakati wa kumeza
Uchovu
Vidonda vinavyouma kwenye kuta za ndani za koo la chakula.
Upasuaji kuondoa sehemu ya koo au koo lote kama limeathirika sana.
Dawa zingine; hutumika kupunguza uvimbe ili iwe rahisi kuundoa kwa upasuaji. Pia huenda zikatumika kutibu. Dawa hizi pia huua chembechembe zingine za mwili na hivyo kupelekea madhara mengine mwilini. Madhara hayo ni pamoja na:
Kupoteza nywele
Kichefuchefu
Kutapika
Uchovu
Maumivu
Magonjwa ya neva za fahamu
Tiba ya asili ya saratani ya koo la chakula
Jambo muhimu ni kumwona daktari na kufanya vipimo unapoona dalili yoyote hatari. Tiba hizi hazina lengo la kuwa mbadala wa tiba ya kawaida lakini kama zikitumika vizuri zinaweza kusaidia.
Kula matunda na mboga mboga kwa wingi sana hasa brokoli na kabeji. Vyakula vingine ni maharage ya soya, ngano nzima, kitunguu saumu.
Vyakula vyenye glutathione kwa wingi kama asparagus, parachichi, zabibu, machungwa na nyanya.
Spirulina huzuia kukua zaidi kwa uvimbe wa saratani.
Pata vitamin A, C, riboflavin na madini ya selenium
Vyakula vya kuepuka kabisa:
Nyama
Mafuta mengi
Chumvi sana
Sukari ya kuongeza
Vyakula vilivyokaangwa sana
Vyakula vya moto au baridi sana
Hoja muhimu za kuzingatia
Uwezekano wa kupona upo kama saratani ikigundulika mapema. Mapema ni bora zaidi.
Saratani ya koo la chakula mara nyingi hugundulika katika hatua za kuchelewa sana. Katika hatua hii haiwezekani kupona bali matibabu ya kukusaidia.
Uwezekano wako wa kuishi ni mkubwa baada ya upasuaji kama saratani haijaenea katika maeneo mengine ya mwili.
Jinsi ya kujikinga na saratani ya koo la chakula
Epuka sigara na matumizi yote ya tumbaku. Dawa na ushauri vipo kukusaidia kuacha matumizi ya vitu hivi. Kama hujaanza, tafadhali usijaribu kuanza.
Epuka pombe
Ongeza matunda na mbogamboga kwenye mlo wako
Kuwa na uzito mzuri wa mwili wako
Epuka matumizi yaliyokithiri ya dawa kama asprin, ibuprofen na naproxen
Neno la tumaini
“Huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu”. 1 petro 5:7
Tuesday, December 18, 2018
SARATANI YA KOO LA CHAKULA
Tags
# AFYA CLICK
About afya
Soratemplates is a blogger resources site is a provider of high quality blogger template with premium looking layout and robust design. The main mission of templatesyard is to provide the best quality blogger templates.
AFYA CLICK
Labels:
AFYA CLICK
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment