Upungufu wa damu (anaemia) hutafsiriwa kama kupungua kwa kiwango cha hemoglobin katika damu damu chini ya kiwango kinachokubalika kiafya. Kiwango cha kawaida cha haemoglobin (Hb) katika mwili wa binadamu ni kati ya gramu 12 mpaka 14 kwa kila mililita ya damu. Hata hivyo shirika la afya duniani (WHO) linatambua kiwango cha mpaka 11gm/mililita kuwa cha kawaida kwa mama mjamzito. Hivyo basi mjamzito mwenye kiwango chochote cha haemoglobin chini ya 11 gm/mililita hutafsiriwa kuwa na upungufu wa damu. Hata hivyo nchi nyingi hasa zinazoendelea hutambua kiwango cha mpaka gramu 10 kwa mililita kuwa ni upungufu wa damu kwa mjamzito.Kwa mjamzito anayehudhuria kliniki kwa mara ya kwanza, upungufu wa damu kipindi cha ujauzito humaanisha kiwango cha hemoglobin chini ya <11.0 g/dL, na mimba inapofikisha wiki 28 upungufu wa damu hutambuliwa iwapo hemoglobin itashuka na kuwa chini ya 10.5 g/dL.
Kwa kuzingatia hilo, mama mjamzito hushauriwa kupima wingi wa damu siku anapohudhuria kliniki kwa mara ya kwanza na pindi mimba inapofikisha wiki 28.
Viwango vya Anaemia
Upungufu wa damu unaweza kugawanywa katika viwango vikuu vinne, yaani upungufu wa damu wa kawaida (mild anaemia) ambao ni kati ya 9-11 gm/ml, upungufu wa damu wa kati (moderate anaemia) ambao ni kati ya 7-9 gm/ml, upungufu wa damu mkali (severe anaemia) ambao ni kati ya 4-7 gm/ml na upungufu wa damu mkali zaidi (very severe anaemia) ambao ni chini ya 4gm/ml.
Mzunguko wa madini ya chuma mwilini
Kwa kawaida mwili wa mwanamke huifadhi gramu 3.5 mpaka 4.5 za madini ya chuma. Asilimia 75 huifadhiwa kama hemoglobin katika chembe damu nyekundu, asilimia 20 kama ferritin katika mifupa na asilimia 5 inayobaki huifadhiwa katika misuli na vimengenyo vingine vya mwili.
Wanawake wasio wajawazito hupoteza karibu gramu 1 za madini ya chuma kutoka katika seli za mwili zinazokufa kila siku na gramu 1 zaidi kila siku wanayokuwa kwenye hedhi.
Ukubwa wa tatizo
Upungufu wa damu kipindi cha ujauzito ni tatizo linalowakumba kina mama wajawazito wengi sana, siyo tu Tanzania bali nchi nyingi zinazoendelea. Inakisikiwa kuwa karibu theluthi moja ya wajawazito katika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito hukumbwa na tatizo hili.
Kwa mujibu wa WHO, inakadiriwa kuwa karibu asilimia 56 ya wajawazito huko kusini mashariki ya Asia hukumbwa na tatizo hili. Kwa hapa Tanzania, hakuna takwimu sahihi kuhusu tatizo hili. Sehemu nyingine duniani, inakadiriwa kuwa karibu asilimia 4-16 ya vifo vinavyotokana na ujauzito husababishwa na upungufu wa damu. Aidha upungufu wa damu wakati wa ujauzito huongeza uwezekano wa madhara kwa mtoto ikiwemo kifo.
Chanzo cha upungufu wa damu wakati wa ujauzito
Kipindi cha ujauzito huambatana na mabadiliko mbalimbali ya mwili. Moja ya mabadiliko hayo ni ongezeko la maji (plasma volume) katika mzunguko wa damu. Katika hali hii, pamoja na kwamba kiasi cha damu huonekana kuongezeka, kiwango cha hemoglobini hupungua mpaka kufikia 11.5mg/dl.
Karibu asilimia 85 ya anaemia wakati wa ujauzito husababishwa na upungufu wa madini ya chuma mwilini. Upungufu wa madini ya chuma unaweza kusababishwa na kula chakula chenye kiasi kidogo cha madini haya au mwili wa mjamzito kushindwa kutunza madini ya chuma ya kutosha kutokana na ama mimba zilizopita au kupoteza kiasi kingi wakati wa hedhi kabla ya kushika mimba.
Vyanzo vingine ni pamoja na
Upungufu wa folic acid
Ugonjwa wa sickle cell
Lishe duni kabla na wakati wa ujauzito
Kupoteza damu kwa sababu ya kuumia au kuwa na minyoo (hookworms)
Ugonjwa wa malaria wakati wa ujauzito
Ugonjwa wa chembe damu nyekundu ujulikanao kama beta thalassaemia. Ugonjwa huu huwapata zaidi watu wanaoishi Asia ya kusini, Ulaya ya kusini na Afrika.
Upungufu wa vitamin B12
Ugonjwa sugu wa kuvunjika chembe damu nyekundu (chronic haemolysis) kama vile ugonjwa kurithi wa chembe damu nyekundu (hereditary spherocytosis)
Ugonjwa wa kupoteza hemoglobin kupitia mkojo (paroxysmal nocturnal hemoglobinuria)
Saratani ya damu (leukemia)
Matatizo ya kupoteza damu kwenye njia ya chakula (gastrointestinal bleeding)
Matatizo katika utumbo hasa wakati wa ujauzito.
Vihatarishi vya tatizo hili
Masuala ya kijamii kama vile umri wa mjamzito, kiwango chake cha elimu na uelewa kuhusu afya yake, kama ana mwenza wa kumsaidia kiuchumi, makazi anayoishi vinaweza kuchangia mjamzito kupata upungufu wa damu
Vihatarishi vingine ni vile vinavyohusu masuala ya uzazi kama vile idadi ya mimba zilizotanguli (waliowahi kuzaa wana hatari ya kupata anaemia kuliko wanaopata mimba kwa mara ya kwanza), kuwa na mimba ya mapacha na kuwa na historia ya kuzaa mtoto njiti
Vihatarishi vingine vinahusu tabia za mjamzito kama vile uvutaji sigara, unywaji wa pombe na kutohudhuria kliniki wakati wa ujauzito
Pia kuwa na magonjwa kama vile kisukari, magonjwa ya figo, pamoja na shinikizo sugu la damu
Sunday, November 25, 2018
UPUNNGUFU WA DAMU KIPINDI CHA UJAUZITO
Tags
# AFYA CLICK
About afya
Soratemplates is a blogger resources site is a provider of high quality blogger template with premium looking layout and robust design. The main mission of templatesyard is to provide the best quality blogger templates.
AFYA CLICK
Labels:
AFYA CLICK
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment